Wednesday, September 11, 2013

OPERETION KIMBUNGA YASABABISHA MMOJA WA WAHAMIAJI HARAMU KUJINYONGA HUKO BUKOBA.

Wakati Operesheni Kimbunga inayoondoa wahamiaji haramu nchini ikiendelea, raia wa Rwanda, France Mathias amejinyonga wilayani Kyerwa, Kagera baada ya mkewe kumgomea kuuza mali na kuondoka nchini.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kitongoji cha Kikukulu wilayani humo ambapo binti yake, Melania, alithibitisha tukio hilo akidai kuwa tangu operesheni hiyo ianze, wazazi wake hao wamekuwa kwenye mzozo mkubwa.
Kutokana na mzozo huo, “baba alitaka wauze mali na kuondoka nchini, lakini mama akampinga na kisha usiku akatoroka na watoto watatu,” alidai Melania na kusema mama yake ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, Tanzania na kwamba kuna wakati baba yao alitishia kuwaua.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikukulu, Joseph Leo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, alithibitisha Mathias kuwa katika orodha ya wahamiaji haramu iliyoandaliwa na uongozi wake na kwamba amekuwa akifahamu kuwapo ugomvi mkubwa ndani ya familia hiyo.
Pia alisema anafahamu baba yake alikuwa na uwezo wa kumiliki kiasi hicho cha fedha ingawa hakufahamu anapozihifadhi na kuwa upo wakati alitishia kuwaua baada ya kuibuka mzozo kwenye familia yao.
Alisema yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliofika juzi kwenye eneo la tukio na kushuhudia Mathias ambaye alifika eneo hilo mwaka 1976 akiwa amejinyonga, huku vipande vya noti za Sh 5,000 na Sh 10,000 zinazokadiriwa kufikia Sh milioni saba vikiwa vimetapakaa chini.
Ofisa Tarafa ya Kituntu, Nicholaus Rugemalira, alisema Mathias alikuwa raia wa Rwanda na kwamba eneo alilojinyongea kulikutwa pia kiberiti na panga hali iliyoashiria kuwa pengine alikuwa na mpango wa kuiteketeza familia yake kwa moto au kuiua kwa panga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alipoulizwa kwa njia ya simu alisema alikuwa hajapata taarifa kamili juu ya tukio hilo ila atafuatilia na kutoa taarifa baadaye.

No comments:

Zilizosomwa zaidi