Sunday, September 22, 2013

MUTUNGI: VYAMA VYA SIASA VISIVYO NA SIFA VIFUTWE

Francis Mutungi

Miaka 21 imepita tangu sheria ya vyama vingi vya siasa ianze kutumika katika nchi yetu. Kama wananchi wengi wanavyokumbuka, Sheria ya Vyama vya Siasa ilianza kutumika Julai 1, 1992 baada ya mikikimikiki mingi ya kisiasa iliyoanzisha safari ndefu ya kuutosa mfumo wa chama kimoja na kuleta mfumo wa siasa za ushindani.
Miaka 21 hakika ni muda mrefu. Kama ilivyo kwa maisha ya binadamu, umri wa miaka 21 ni mkubwa na ndio maana Katiba yetu inamtambua mtu aliye na miaka 18 na kuendelea kama mtu mzima. Hivyo, miaka 21 ya uhai wa vyama vya upinzani vilivyoanzishwa kuingia katika ushindani wa kisiasa na CCM, inatosha kabisa kwa vyama hivyo kukomaa na kujiendesha kwa mujibu wa sheria zilizopo pasipo kubebwa kwa mbeleko ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Lazima tukiri kwamba mwanzo wa mfumo huo wa vyama vingi ulikuwa mgumu, kwani mfumo wa chama kimoja haukuweza kufutika kirahisi kutokana na CCM kutojitayarisha kisaikolojia kabla mfumo wa vyama vingi haujaanza kutumika. Hivyo, Msajili wa kwanza, George Liundi alipata wakati mgumu kuvilea vyama hivyo vichanga, huku akiyumbishwa na viongozi wa CCM na serikali yake ambao walikuwa wagumu kukubali mabadiliko hayo ya kihistoria.
Kwa kiasi kikubwa, chama hicho kiliendelea kutumia vyombo vya ulinzi na usalama, hasa Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa katika kukabiliana na vyama vya upinzani. Mfumo wa chama kimoja ulivibadili vyama vya Tanu na Afro-Shirazi (na baadaye CCM), kutoka kuwa vyama vya siasa na kuwa vyama vya dola. Kutokana na hali hiyo, viongozi wa vyama vya upinzani walidumaa kutokana na kufanya siasa katika mazingira hatarishi ya kupigwa na kufunguliwa mashtaka ya uongo katika vyombo vya sheria.
Msajili John Tendwa alipomrithi Liundi alikuta hali ikiwa bado ngumu na tete. Msajili huyo mpya alishindwa kujikwamua katika makucha ya chama hicho tawala na aliendelea kuwa mateka wa mfumo hasi wa chama kimoja. Taratibu CCM kwa kiasi fulani ilianza kukubali mabadiliko, ingawa iliendelea kutegemea Jeshi la Polisi kukwamisha mikakati na shughuli za wapinzani kama mikutano ya hadhara na maandamano.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alilazimika mapema mwaka huu kukionya chama chake hicho kuwa, kutokana na mazingira ya sasa hakitaweza tena kulitegemea Jeshi la Polisi katika kufanya shughuli zake za kisiasa. Tamko hilo ni uthibitisho tosha kwamba Msajili mpya, Jaji Francis Mutungi anaingia ofisini kufanya kazi zake katika mazingira mazuri. Pengine ndio maana mwishoni mwa wiki alikuwa na ujasiri wa kutoa karipio kali kwa chama tawala kwa kumtumia Balozi wa China nchini kwa shughuli za kisiasa kinyume na sheria za nchi yetu na Mkataba wa Kimataifa wa Vienna.
Sasa tunayo kila sababu ya kusema kuwa, Jaji Mutungi hatakuwa na kisingizio chochote cha kushindwa kusimamia kikamilifu sheria hiyo ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Hatakuwa na kisingizio cha kutounga mkono vyama vyenye sifa ambavyo vinafanya shughuli za kisiasa kikamilifu kama CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kama ambavyo hatakuwa na kisingizio cha kutovifuta vyama pandikizi na vya mifukoni vinavyojiita vyama vya siasa pasipo kufanya kazi za kisiasa.

No comments:

Zilizosomwa zaidi