Tuesday, September 24, 2013

MOYES AIPIGIA SALUTI MAN CITY

Kocha David Moyes amekiri kwamba watani zao, Manchester City, waliwazidi kila kitu kabla ya kuwafunga mabao 4-1 katika mechi ya juzi Jumapili katika Uwanja wa Etihad, lakini akaahidi kwamba watarudi katika makali yao haraka iwezekanavyo.
Moyes alishuhudia bao pekee la Wayne Rooney likijaribu kuifariji timu yake ya Manchester United mwishoni mwa mchezo, lakini mabao mawili ya Sergio Aguero na mengine mawili ya Samir Nasri na Yaya Toure yalishamkata maini.
“Hatukucheza vizuri. Walikuwa bora kuliko sisi. Walianza wakiwa imara na walikuwa wepesi kuliko sisi. Tutarudi tukiwa imara, msimu bado mrefu. Tutakiweka kipigo hiki nyuma yetu na kusonga mbele,” alisema Moyes.
“Nadhani Manchester City walikuwa wazuri sana. Hatukuwa wazuri, lakini pia City walianza mechi vizuri sana, tungeweza kurudi vyema katika kipindi cha pili kama wangeongoza kwa bao 1-0 lakini kwa kufungwa bao la pili kabla ya kwenda mapumziko kulileta mabadiliko makubwa. Kisha walikuja kipindi cha pili wakiwa imara zaidi.”
Moyes alikiri kwamba Manchester City ilikuwa timu bora zaidi katika mechi hiyo ya watani wa jadi wa Jiji la Manchester, lakini timu yake itaimarika zaidi siku za usoni. “Nadhani walipata moto wa mechi mapema zaidi, sisi hatukuweza kufanya hivyo. Hatukuweza kabisa kukabiliana na viungo wao mapema katika mechi hii, kwa sababu hiyo walianza kutawala mechi. Ilibidi tuwe imara lakini hatukuweza kumudu,” alikiri.
Alipoulizwa kuhusu kiwango binafsi cha Rooney, Moyes alijikuta akimsifia nyota huyo ambaye mwanzoni mwa msimu aliwahi kukaririwa akisema kwamba angekuwa mchezaji wa pili.
“Naweza kusema kiwango chake leo (juzi Jumapili) kimekuwa kizuri sana. Hakustahili kuwa upande wa timu iliyofungwa. Alikuwa katika kiwango cha juu na alikuwa katika daraja la kwanza,” aliongeza  Moyes.
Manchester United imepata pointi saba katika mechi zao tano za mwanzo huku ikishindwa kuondoka na pointi tatu katika mechi tatu kubwa dhidi ya Chelsea, Liverpool na Manchester City. Moyes amerudia tena kulia kuwa Man United imepewa mwanzo mgumu.
“Tulisema kuwa ulikuwa mwanzo mgumu. Nilisema wakati ule, jinsi ratiba ilivyojitokeza ilikuwa kama vile imepangwa. Mpaka sasa nashawishika kuamini hivyo,” alisema.
Mwanasport

No comments:

Zilizosomwa zaidi