Rais Jakaya Kikwete |
Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea
Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za
kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward
jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya
dawa ya kukamatwa na dawa hizo.
Rais Kikwete alisema Serikali yake itakabiliana na
biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume na sheria
za nchi.
Alisema hayo juzi usiku alipokutana na Watanzania
wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani...“Serikali yangu
haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya na
kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria za
nchi yetu.”
Masogange na Melisa walikamatwa Julai 2, mwaka huu
kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha
kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache baada ya meli ya
mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na
askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya
Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye
thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Pia, Agosti 31, mwaka huu, mshambuliaji nyota wa
zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na
bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis
Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba
dawa za kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania
wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika
nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa
sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi
kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho.
Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa.
Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei
kamwe,” alisema.
Masogange, Melisa wakosa dhamana
Masogange na mwenzake Melisa jana walikosa dhamana
baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North Gauteng,
Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika
kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza kuwa,
Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena
Novemba mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha
Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao
walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha
dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.
Awahoji akina Masogange
Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini kuwahoji
Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema
hawakumpa ushirikiano.
Kamanda huyo alisema imebainika kuwa mzigo
walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali
zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai
hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea
kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa
za Kulevya cha Afrika Kusini.
Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.
No comments:
Post a Comment