Wednesday, September 18, 2013

BALALI ATAJWA KATIKA KESI YA MRAMBA NA YONA

 
Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hayati Dk. Daudi Balali ametajwa kuwa ndiye aliyeialika na kuiongezea mkataba wa ukaguzi wa madini nchini Kampuni ya Alex Stewart.

Ushahidi huo ulitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na aliyekuwa Mkurugenzi wa Soko la Fedha wa BoT, Crecencia Mbatia (61), ambaye anamtetea aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba.

Mbatia ambaye alikuwa mwenyekiti wa timu ya watu watano ya majadiliano ya jinsi ya kupata kampuni hiyo na wenzake, kisha kuandaa mkataba kati ya BoT na Alex Stewart, alisema kuwa Dk. Balali ndiye alitoa idhini na sio Mramba wala aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Mramba, Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gragy Mgonja wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 kutokana na Kampuni ya Alex Sterwart kupewa msamaha wa kodi bila ridhaa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji John Utamwa, Sam Rumanyika na Hakimu Mkazi Saul Kinemela.

Mbatia alidai kuwa hivi sasa ni mstaafu, lakini mwaka 2002 akiwa na wadhifa huo aliongoza timu hiyo ya majadiliano vizuri na kwamba ilifanya kazi ya kumtafuta mkaguzi wa madini kupitia intaneti.

Aliongeza kuwa wakati wanatafuta kampuni hizo, walizipata 21, lakini kamati yake ilichagua tano na serikali kupitia BoT ikaziandikia barua zije kwenye majadiliano.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, kampuni mbili tu ndizo zilijibu barua ya serikali ikiwemo Alex Stewart na baada ya mchakato, ikakubaliwa kuja nchini kufanya kazi hiyo.

Mbatia ambaye alikuwa akiongozwa na wakili wa kujitegemea, Herbbet Nyange kutoa ushahidi wake, alidai kuwa katika kipindi chote cha kamati ya awali aliyokuwa akiiongoza hapakuwepo mwakilishi toka Wizara ya Fedha.

Aliongeza kuwa alikuwa akiwaona wanasheria toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao walikuwa wakishiriki katika vikao vya timu hiyo ya majadiliano.

“Hata hivyo, timu yangu haikuweza kufanya majadiliano na Kampuni ya Alex Stewart kwa sababu wakili wake alivyofika katika timu yangu alisema haoni haja ya kufanya majadiliano kuhusu bei na gharama za uendeshaji na timu hiyo, kwani tayari Gavana Balali kwa niaba ya BoT na serikali nzima ilikuwa tayari imeishamtumia barua ya mwaliko ikionyesha jinsi atakavyofanya kazi na gharama za uendeshaji,” alieleza.

Mbatia alijibu maswali aliyokuwa akiulizwa na wakili wa Yona, Elisa Msuya huku akisoma kielezo cha 11 ambacho ni barua ya BoT kwenda kwa kampuni hiyo, ambayo Gavana Balali aliiandikia kuiarifu kuwa imeiongezea tena mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, upande wa jamhuri unaongozwa na wakili wa serikali, Oswald Tibabyekomya na Shadrack Kimaro uliomba mahakama iahirishe kwa muda kesi hiyo ili waweze kwenda kujiandaa na maswali ya kumuuliza shahidi huyo.

Jaji Utamwa aliahirisha kesi hiyo hadi leo shahidi huyo atakapokuja kuhojiwa na upande wa jamhuri.

Novemba 2008 ilidaiwa mahakamani hapo na mawakili wa upande wa jamhuri kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya matumuzi mabaya ya madaraka na kuisasababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
Tanzania daima

No comments:

Zilizosomwa zaidi