Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata askari wake 16 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kushiriki na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa magendo wanaovusha bidhaa zao kupitia bandari bubu kandokando ya Bahari ya Hindi na maeneo mengine.
Hatua hiyo umekuja baada ya kubaini baadhi ya
askari wa vikosi mbalimbali ambao imeelezwa kuwa wametengeneza mtandao
huo ulioanzishwa zaidi ya miezi sita kwa kushirikiana na baadhi ya
wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao hukusanya fedha
kinyume cha sheria kutoka kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru
halali Serikalini.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema: "Tumeshirikiana na wananchi kwa kufuatilia nyendo
za askari hao na kubaini kuwa walitengeneza mtandao huo wa kuvusha mali
kupitia bandari bubu zisizo rasmi maeneo ya Kawe hadi Bagamoyo."
Alisema polisi kupitia teknolojia ya kisasa
iliwabaini askari hao kwa nyakati mbalimbali wakishirikiana na
wafanyabiashara hao ambao walikuwa wakitoa rushwa ili wasikamatwe.
“Mpaka sasa askari wa vyeo mbalimbali waliokamatwa
wako 16 na wanaendelea kuhojiwa... majina yao yanahifadhiwa kwa sasa
kwani bado kuna wengine wanatafutwa ili kuwabaini na kuusambaratisha
mtandao mzima,” alisema.
Alisema mtu yeyote ambaye amefanya kosa ndani ya
Jeshi la Polisi atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani
kama raia wengine.
Kamanda Kova alisema operesheni hiyo itawalenga
wafanyabiashara, wafanyakazi wa TRA na wa taasisi nyingine
watakaobainika kuhusika na mtandao huo.
No comments:
Post a Comment