Monday, April 29, 2013

SIMBA YAJIPANGA UPYA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope ameanza kazi rasmi na leo, Jumamosi atakuwa na vikao mfululizo kuweka mikakati ya kumaliza ufalme wa Yanga.

Hanspope, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Friends of Simba, tayari ameanza vikao na wajumbe wa kundi hilo na vitaendelea leo Jumamosi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hanspope ambaye alirejea katika nafasi hiyo katikati ya wiki hii baada ya kumaliza tofauti zake na uongozi wa Simba, alisema wikiendi hii atakuwa na vikao mfululizo na wadau wengine ili kuweka mikakati ya kuijenga klabu hiyo ya Msimbazi.
Kutokana na amani iliyopo sasa, naamini mambo yatakwenda vizuri na tutapata ushindi katika mambo yetu. Waliojitoa wengi wamerudi na wengine watarudi, alisema Hanspope.

Ingawa, Hanspope hakuweka wazi, Mwanaspoti linajua kuwa atakuwa na mkutano na wanachama wa Kundi la Friends of Simba ili kupanga mikakati ya mechi dhidi ya Yanga, Mei 18 mwaka huu.

Ajenda nyingine zitakuwa ni kupanga mikakati ya usajili na kujadili mahali pa kuiweka kambi timu yao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hanspope, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji alisema ili Simba ipate maendeleo jambo la muhimu ni kuwa na amani.
Zawadi ya amani ni ushindi, zawadi ya migogoro ni kufanya vibaya kama tulivyoona sasa, alisisitiza kapteni huyo mstaafu wa jeshi.

Akiuzungumzia usajili wa msimu ujao, alisema watakuwa makini sana katika hilo, kwani msimu uliopita walifanya usajili wa pupa na wa bei mbaya ambao haujawasaidia.
Tulisajili wachezaji wa bei ya juu lakini hawakutusaidia, mathalani wachezaji wa nje waliotusaidia ni kipa Abel Dhaira na Emmanuel Okwi, ambaye tayari tumemuuza, alisema Hanspope.

Hanspope na baadhi ya wanachama wa Kundi la Friends of Simba walijitoa na wengine kususa kuisaidia timu hiyo kwa kilichodaiwa kuwa ni kutokubaliana na uongozi.
          

No comments:

Zilizosomwa zaidi