Thursday, April 11, 2013

KILICHOANDIKWA NA GAZETI LA MWANANCHI KUHUSU SUMATRA KUKAMATA DALADALA ZILIZOPANDISHA NAULI...!

 
Dar es Salaam.Wakati nauli mpya zikianza kutumika leo huku Serikali ikizibariki, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) imekamata magari ya kubeba abiria (daladala) 75 katika operesheni maalum iliyoanza mwanzoni mwa wiki hii mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Uamuzi wa kukamata magari hayo umekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya abiria ya madai ya kutozwa nauli kubwa kuliko iliyotangazwa na Serikali kuwa zianze kutumika leo.

Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe alisema jana mjini Dodoma kuwa ongezeko la viwango vipya vya nauli si tatizo, la muhimu ni wahusika kufuata vigezo.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shio alisema kuwa,daladala zilizokamatwa zilikuwa na makosa mbalimbali yakiwemo kukatisha ruti, kutoza nauli, kuiba ruti na kufanya biashara ya kusafirisha abiria bila ya kuwa na kibali.

Alisema kutokana na hali hiyo wamiliki wa daladala zilizokamatwa wametakiwa kwenda na mikataba ya madereva wapya, ili wale wa zamani waweze kukaguliwa na Jeshi la Polisi Tanzania juu ya uhalali wa leseni zao.

“Tumepata malalamiko ya daladala 105 ambazo zimekuwa zikivunja sheria ya usafiri barabarani, ambapo daladala 75 tayari tumezikamata,” alisema Shio.
Aliongeza kati ya hizo, daladala 36 zilikatisha ruti, wakati 18 ziliiba ruti na 21 zilitoza nauli kubwa, jambo ambalo limewafanya wazichukulie hatua.
Alisema kuna nyingine zimebeba abiria bila ya kuwa na kibali, ambapo wamiliki wake wamechukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kutokana na hali hiyo, wamiliki wa daladala hizo wametakiwa kulipa faini na kwenda na mikataba ya madereva wapya ili madereva waliofanya makosa wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani. Alisema daladala ambazo zilikuwa zinafanya kazi bila ya kibali hasa nyakati za usiku katika baadhi ya maeneo zimepelekwa kwenye yadi ya Serikali ili wamiliki wake waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu ni kosa kubeba abiria wakati huna kibali cha usafirishaji.

Alisema kuwa, ili kupunguza ukubwa wa tatizo, wamelifanya zoezi hilo kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwataka madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kupunguza malalamiko. Alisema kutokana na hali hiyo Sumatra itaendelea kukamata magari ambayo yataonekana yanaendelea kuvunja sheria kwa makusudi.

No comments:

Zilizosomwa zaidi