Hali ya afya ya Mkuu wa Usalama na Ulinzi wa
Chadema, Wilfred Lwakatare anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma
za kuwahamasisha watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia
mitandao ya jamii, imezorota.
Wakili wake Nyaronyo Kicheere, amelalamikia hali yake kuwa si njema
kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao.
Alikuwa akitembea kwa kujivuta, na alidai kuwa ameshindwa kula chakula inavyotakiwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakili
Kicheere alisema amehangaika sana katika kuhakikisha kuwa mteja wake
anapata dhamana lakini imeshindikana, hali ambayo inamtia hofu kutokana
na hali aliyomwona nayo.
“Mteja wangu ni mgonjwa wa kisukari, kwa kawaida
hutakiwa kula chakula na kunywa maji mengi, lakini nimehangaika sana,
leo (jana) nilikuwa na matumaini kwamba atapelekwa mahakamani ambapo
nilijipanga kwa kuandaa watu makini wenye hati za nyumba nikiwa na imani
kwamba angepata dhamana, lakini wamemrudisha mahabusu,” alisema
Kicheere.
Kicheere muda mwingi alionekana kuhaha kuwasiliana
na viongozi wa Chadema kwa simu yake ya mkononi, pamoja na kuwasiliana
na baadhi ya wanasheria akiwamo Tundu Lissu na Peter Kibatala ambao
walijipanga katika kuhakikisha kuwa wanapata wadhamini watakaoweza
kumdhamini Lwakatare.
Wakili huyo alisema kuwa kinachotendeka kwa mteja wake ni kinyume cha sheria kwa kuwa ni tuhuma ndizo zimemfanya akamatwe.
Alisema mteja wake ana haki ya kupewa dhamana hasa
kwa kuzingatia kuwa saa zaidi ya 24 zimepita na hali yake si njema, na
kwamba kuendelea kuwa mahabusu ni kuhatarisha usalama wa afya yake.
Maofisa wa juu kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa
Upelelelezi wa Makosa ya Jinai, waliwasili Kituo Kikuu cha Polisi jijini
Dar es Salaam ambapo walikutana na wakili Kicheere na mtuhumiwa huyo na
kufanya mazungumzo.
Taarifa za kuaminika zilizopatikana awali
zilieleza kuwa juzi saa 11 jioni maofisa kadhaa wa polisi, walimchukua
mtuhumiwa huyo na kwenda naye nyumbani kwake wakiwa na lengo la kufanya
upekuzi kwa mara ya pili lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya
kutokuwa na kibali cha upekuzi.
“Wakili wake anawabana maofisa wa polisi akitaka
wafanye kazi zao kwa mujibu wa sheria hivyo juzi hawakuweza kuingia
ndani, pia walizuiwa na wakili huyo huyo kumhoji kwa kumrekodi kwa
video, ambapo kulitokea hali ya majibishano ya kisheria, lakini hatimaye
akahojiwa bila kurekodiwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lwakatare alikamatwa Jumatano ya wiki hii katika
makao makuu ya chama hicho na tangu siku hiyo anaendelea kushikiliwa na
polisi kwa mahojiano.
Chanzo Mwananchi gazeti.
Chanzo Mwananchi gazeti.
No comments:
Post a Comment