Wednesday, December 12, 2012

STORI YA NGASSA KUHAMIA SUDANI IKO HAPA......KWA HABARI ZAIDI INGIA HAPA

VIONGOZI wa Simba na Azam wamesema uamuzi wa winga Mrisho Ngassa kugoma kwenda kufanyiwa vipimo vya afya kama hatua ya awali ya kujiunga na klabu ya El-Merreikh ya Sudan imeiaibisha nchi.
Mbali na kuiaibisha nchi, klabu hizo kwa pamoja zinaona kitendo hicho kuwa ni utovu wa nidhamu na usumbufu kwa viongozi wa timu hiyo ya Sudan waliokuja nchini kukamilisha zoezi hilo.
Simba na Azam zilitangaza kukubaliana kumuuza Ngassa kwa ada ya Dola 100,000 (Sh157 milioni). Katika makubaliano ya mkataba wa mchezaji huyo, El Merreikh ilidaiwa kuwa tayari kumpa Ngassa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Dola 75,000 (Sh118 milioni).
Jana alipaswa kufanyiwa vipimo vya afya jijini Dar es Salaam chini ya viongozi wa timu hiyo ya Sudan, lakini katika hali ya kushangaza hakutokea.
Akikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari juzi, Ngassa alisema hayuko tayari kujiunga na El Merreikh kwa vile siyo Simba wala Azam iliyomshirikisha katika zoezi hilo.
Hata hivyo kauli ya Ngassa inapingana na aliyoitoa wakati akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa Bara (Kilimanjaro Stars), akiitaka Simba iache kumbania kuchezea timu hiyo ya Sudan.
Makamu Mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange alisema wamesikitishwa na kitendo alichofanya Ngassa na kwamba watamwita ili kumhoji.“Hatufahamu nini kimempata mpaka sasa. Kwanza hao viongozi wa El Merreikh yeye binafsi ndiye aliyeongea nao na kufikia makubaliano,” alisema Nyange.
Nyange alisema wameshangazwa na uamuzi wa Ngassa wa kubadilika ghafla. “Pengine kuna kitu hapa, amebadilika ghafla,” aliongeza Nyange aliyeteuliwa kuzungumzia suala hilo pia kwa niaba ya Azam.
Alisema kitendo hicho kimeiaibisha Simba na Taifa kwa jumla kwani ni sawa na kuwafungia milango wachezaji wengine wenye nia ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Wakati huohuo, Juma Nyoso ameendelea kuisisitizia klabu yake ya Simba kusitisha mkataba wake haraka ili ajiunge na timu ya Coastal Union ya Tanga.
Uongozi wa Simba ulimpeleka Nyoso kujifua na kikosi cha timu ya vijana kwa madai ya kushuka kiwango na utovu wa nidhamu.Hata hivyo beki huyo anayecheza nafasi ya kati, aligoma kutekeleza agizo hilo la kwenda kujiunga na kikosi B.
CHANZO; MWANANCHI GAZETI

No comments:

Zilizosomwa zaidi