
Kampuni
za simu za mkononi za Tigo, Airtel na Zantel zimeunganisha huduma zao
za kutoa, kutuma na kuweka fedha na sasa mteja anaweza kutuma fedha
kutoka mtandao mmoja kupitia mwingine.
Taarifa ya pamoja na kampuni hizo iliyotolewa jana, ilisema kuwa wote
wanaotumia huduma za kifedha za mitandao hiyo, wataweza kutumiana fedha
kupitia simu zao za mikononi pasi na tatizo baada ya kampuni hizo
kuunganisha huduma zao.
Huduma hiyo inayotarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi huu,
itawafanya wateja wa mitandao hiyo kutumiana na kupokea fedha moja kwa
moja kwenye akaunti zao tofauti na ilivyokuwa awali.
Taarifa hiyo ilisema ushirikiano huo unaweka rekodi ya hatua muhimu
katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini na Afrika kwa kuwa si
rahisi kwa kampuni zinazoshindana kufanya uamuzi wa kibiashara wa aina
hiyo.
“Ikumbukwe kuwa makubaliano ya namna hii hapo awali yalifanywa na
kampuni za simu kuwawezesha wateja wao kupata huduma za kupigiana simu
na kutumiana ujumbe mfupi pekee,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya
pamoja na kuongeza kuwa, wateja wao watapata pia punguzo la gharama za
uhamishaji fedha, pia hawatahitajika kuwa na namba ya siri.
Kwa sasa, ili mteja aweze kupokea fedha alizotumiwa kutoka mtandao
mwingine, anahitajika kuonyesha namba ya siri (pin) wakati wa kutoa
fedha jambo ambalo limekuwa likitatiza ufanisi wa miamala hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose alisema kampuni hizo zina
dhamira ya dhati kuhakikisha huduma na ushirikiano huo vinawawezesha
wateja kufanya biashara zao kwa ufanisi na urahisi zaidi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez alisema anafurahi kushirikiana
na washindani wake, Airtel na Zantel katika jitihada za kuendeleza
huduma za kutuma na kupokea fedha kupitia simu za mkononi nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Sunil Colaso alisema kampuni yake imejikita
katika kuwapa wateja wake huduma zenye ubunifu wa hali ya juu bila
kujali ushindani wa kibiashara.
Matumizi ya simu za mkononi kufanya miamala ya kifedha yamezidi kukua
kwa kasi nchini na kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa hadi sasa kuna watumiaji wa huduma za
fedha kwa simu za mkononi 12,330,962.
No comments:
Post a Comment