Wakati viongozi wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiweka kambi Zanzibar, Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana naye alitumia siku nzima
visiwani humo akikutana na baadhi ya viongozi wa Serikali, katika kile
kinachotafsiriwa kuwa kulinusuru Bunge hilo.
Habari zilizolifikia gazeti hili
kutoka Zanzibar zinasema Sitta alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais
Mstaafu, Aman Karume na mwanasiasa wa siku nyingi wa CCM, Mzee Hassan
Nassor Moyo.
Zanzibar kwa sasa ndiyo moyo wa
upatikanaji wa Katiba Mpya kutokana na wajumbe wake katika Bunge
kutegemewa ama kuipitisha au kuikwamisha kwa kuwa kila upande kati ya
mbili zinazovutana, hauna uhakika wa kupata theluthi mbili za kura.
Baada ya kuondoka bungeni na kutangaza
kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, siku mbili baadaye
viongozi wa Ukawa waliingia Zanzibar wakitaka kufanya mikutano ya
hadhara kuwaeleza wananchi sababu za kufanya hivyo, lakini wakazuiwa na
polisi na hadi jana walikuwa wanasubiri kibali.
Safari ya Sitta
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis
Hamad pamoja na kuthibitisha ziara ya Sitta Zanzibar kuwa alikuwa
akutane na Dk Shein, alisema hafahamu lolote kuhusu mkutano wake na
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
"Sifahamu malengo ya safari wala
walichokwenda kuzungumza, ila ni kweli kwamba alifika Zanzibar leo
(jana) na alitarajiwa kuondoka jioni kurejea Dodoma," alisema Hamad na
kuongeza:
"Hilo la kuonana na Maalim Seif
silifahamu ila ninachojua aliniambia nimfanyie miadi ya kuonana na Dk
Shein na nikaifanya kama alivyoelekeza."
Mapema habari zilizolifikia gazeti
hili kutoka Zanzibar zilisema, Sitta baada ya kukutana na Karume, Shein
na Mzee Moyo alitarajiwa kukutana na Maalim Seif saa 9:00 alasiri.
Katibu wa Maalim Seif, Issa Kheri
Hussein alithibitisha kwamba Sitta alikutana na kiongozi huyo nyumbani
kwake, Mbweni saa 9:30 alasiri jana, lakini alidai kutokuwa na taarifa
za mazungumzo hayo.
"Hilo naweza kulithibitisha kwamba
mkutano huo umefanyika lakini mazungumzo yenyewe yalikuwa ya faragha na
mimi baada ya Sitta kufika niliondoka, hivyo sikuweza kufahamu
kilichozungumzwa kwa undani, pengine mpaka nizungumze na Maalim
mwenyewe," alisema Hussein.
Ziara ya Sitta kwenda Zanzibar imekuja
wakati ambao kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa kukwama kwa vikao vya Bunge
hilo kutokana na msimamo wa Ukawa.
No comments:
Post a Comment