Sunday, January 12, 2014

DAWASCO YADAI BILLION 40, YAKATIWA UMEME NA TANESCO


Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), imesema inawadai wateja sugu Sh40 bilioni huku ikiwataka kulipa madeni hayo ili kunusuru utendaji wake.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya mamlaka hiyo kukatiwa huduma za umeme kutokana na kudaiwa Sh6.3 bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza ofisini kwake, Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Jackson Midala alisema deni hilo linahusisha baadhi ya taasisi mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
“Kuna Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na wangine wengi, hatutawakatia huduma kwa sababu ya madeni ila tunasisitiza kulipa madeni hayo ili na tuweze kulipa mzigo wa madeni mengine ya umeme,” alisema Midala.
Pia, Midala alisema kuhusu hatua zinazoendelea kuwashughulikia wateja wanaoiba maji kwa njia za kuharibu mita na kwamba, mpaka sasa wamefanikiwa kuwakamata watu 284 na kuwafikisha mahakamani.
Alisema miongoni mwa watu hao, watatu walihukumiwa adhabu ya kifungo, watatu kesi zilifutwa kwa kukosa ushahidi na wengine kesi zao zinaendelea.
“Wahalifu hao kuna vigogo na watu wa kawaida ingawa baadhi yao walikuwa wanakiri mapema na kulipa faini, kwa mfano Kampuni ya Struberg inayojenga barabara tuliwakamata wakiiba maji yetu wakakiri na kulipia faini ya Sh27 milioni,” alisema Midala.
Aliwataka wateja kulipa ankara zao kwa muda, lengo likiwa ni kuwezesha mamlaka hiyo kujiendesha na kuendelea kuwapa huduma.
Chanzo: Mwananchi

No comments: