Saturday, November 2, 2013

TANZANIA DAIMA: YA LOWASSA YAMNYEMELEA PINDA, KAMATI TEULE YAZUA HOFU

Waziri Mkuu, Mizengo pinda
Hofu ya kung’oka kwa mawaziri wasiopungua watano akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imeanza kushika kasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili limebaini.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba, huenda safari hii usiwe upepo unaopita tu bila madhara, bali kikawa kimbunga cha kuwaondoa madarakani mawaziri hao kwa madai ya kushindwa kuwajibika.

Pinda na mawaziri wenzake, Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) wanashinikizwa kujiuzulu.

Mawaziri hao juzi walishambuliwa na wabunge kuwa taasisi na watendaji walio chini yao wameendesha operesheni za kupambana na ujangili na kuhamisha mifugo zilizosababisha vifo, ubakaji, majeruhi na uharibifu wa mali kwa wananchi wasio na hatia.

Tayari Bunge limepitisha azimio la kuunda kamati teule ambayo inatarajiwa kutangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, bungeni kesho.

Hatua ya kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kumekitia hofu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho tangu mwaka 2008 kimekuwa kikihaha kutibu majeraha ya makundi yanayohasimiana yanayodaiwa kushamiri mara baada ya Edward Lowassa kujiuzulu.

Majina ya kamati teule yanayotarajia kutangazwa kesho, ndiyo yatakayotoa picha ya mwelekeo wa siasa za chama hicho.

Iwapo kamati teule ikibaini tuhuma walizotoa wabunge,  za watu kubakwa, kuuawa, kuteswa, ng’ombe kupigwa risasi, wafugaji kutozwa faini kubwa, kulazimishwa kuuza mifugo yao kwa bei ndogo, Pinda na mawaziri wenzake waliotajwa watalazimika kujiuzulu au rais kutengua uteuzi wao.

Wadadisi wa mambo ya siasa wanadokeza kuwa kuendelea kuwapo madarakani kwa Pinda kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye mara kwa mara amekuwa akimkingia kifua licha ya kupelekewa malalamiko ya utendaji hafifu wa Pinda.

Baadhi ya makada waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, wamedokeza kuwa kitendo cha wabunge kuunda kamati teule ya kuchunguza migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hakitamnusuru Pinda.

Makada hao wanasema Pinda hawezi kuepuka kimbunga hicho kwa madai kuwa baadhi ya wabunge na hata mawaziri hawaridhishwi na utendaji wake, hivyo matokeo ya tume hiyo yatatoa fursa ya azima yao ya siku nyingi ya kutaka kumng’oa madarakani.

Rais Kikwete ndiye tegemeo pekee la kusalia madarakani kwa Pinda anayedaiwa kushindwa kuimudu ofisi hiyo iliyoachwa na mtangulizi wake, Lowassa, aliyejiuzulu Februari mwaka 2008, baada ya kuguswa na kashfa ya Richmond.

Historia ya kamati inaonyesha kuwa ripoti zake mara nyingi zimesababisha kujiuzulu au kuondolewa madarakani kwa watu wanaoguswa nazo.

Mtangulizi wa Pinda ambaye ni Mbunge wa Monduli, Lowassa, alilazimika kuondoka madarakani baada ya ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, kubaini kulikuwa na upendeleo katika zabuni iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond.

Pinda inadaiwa amekuwa si mtoaji maamuzi kwa masuala yanayowagusa watendaji walio chini yake, hivyo kuathiri utendaji kazi wa serikali.

Kama Pinda atajiuzulu, Rais Kikwete atalazimika kuunda baraza jipya la mawaziri ambalo litakuwa la nne tangu aingie madarakani mwaka 2005.

Rais Kikwete aliunda serikali mwaka 2006 mara baada ya kuingia madarakani lakini Aprili 2008 alifanya mabadiliko baada ya Lowassa kutuhumiwa na kamati teule iliyoundwa kuchunguza kashfa mbalimbali zilizohusu kampuni za kuzalisha umeme.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 Rais Kikwete alifanya mabadiliko kwa mara ya pili, baada ya kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili, huku waliokuwa mawaziri 2005-2010 wakiangushwa katika kinyang’aro cha ubunge kwenye majimbo yao.

Kikwete alifanya mabadiliko mengine Mei mwaka jana, mabadiliko yaliyomwacha aliyekuwa Waziri wa Fedha Mustapha Mukulo,  aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami,  aliyekuwa Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.

Waziri mmoja wa zamani anasema wabunge watakaoteuliwa na Spika kuunda kamati teule wanaweza kutumia mwanya wa makundi ya kisiasa kumwajibisha Pinda na wenzake kwa lengo la kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi wa rais mwaka 2015.

Historia za kamati teule
Historia inaonyesha kuwa kila kamati teule ilipoundwa haikuwaacha salama watuhumiwa, ikiwa ushahidi utatolewa wa kutosha. Juzi Spika Makinda aliafiki wazo la kuundwa kwa kamati teule.

Hata hivyo kamati teule hizo kila zinapoundwa na ripoti yake kusomwa zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani kwa watendaji mbalimbali.

Februari 8, 2008, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond kumgusa.

Mwaka juzi, Bunge liliunda kamati teule kuchunguza matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa kuchangisha sh milioni 50 kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara, ili kufanikisha upitishwaji wa bajeti, na ripoti yake ilimng’oa Katibu wake, David Jairo.

Mvutano
Wakati hofu hiyo ikitanda Bunge limegawanyika katika suala hili, kukiwapo mvutano mkubwa kama mawaziri hao wawajibishwe au la, licha ya mawaziri hao kutoa kauli za serikali na kuomba radhi ili wahusika waweze kuwajibishwa.

Tayari Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amejitokeza na kusema hoja yao imetekwa na Spika wa Bunge, Makinda, na kuifanya ni ya kwake na si ya wabunge waliotoa hoja.

“Hoja imechukuliwa na Spika, akaanza kuamua baadhi ya mambo yaanze kuchunguzwa na Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo imeteuliwa na yeye, tulitegemea tupewe fursa ya kuhitimisha hoja zetu kisha  iundwe kamati teule kutegemea hadidu za rejea za wabunge, lakini kwa utaratibu uliofuatwa na Spika, watoa hoja hatujapewa nafasi ya kuhitimisha hoja zetu,”  alilalamika Lugola.

Lugola aliongeza kwamba damu zilizomwagika hazitaenda bure, watu wakileta majibu mepesi yasiyowawajibisha Pinda na wenzake hatakubali, maana wananchi wameuawa, wamebakwa, wameteswa, ng’ombe wakauawa kwa kupigwa risasi, kama kuna mbunge asiyewapenda Watanzania apeleke utetezi kwa masuala hayo mazito.

Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alisema kila chama kilichoko madarakani kinapenda kutawala, hivyo mawaziri waliozembea iwapo hawatachukuliwa hatua chama kinachoongoza kinajiandalia anguko katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo baadhi ya wabunge wa chama tawala wanaona haikuwa busara kwa Spika Makinda kuruhusu hoja ya kuundwa kwa kamati teule, hasa katika kipindi hiki ambapo vyama vya upinzani vimeonekana kuimarika zaidi.

Kuimarika kwa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kumechangia makada wa CCM kujawa na hofu ya kile kitakachogunduliwa na kamati teule.

Wabunge hao walisema hivi sasa bado chama chao hakijapata uungwaji mkono katika mchakato wa sheria ya Katiba mpya, hivyo kamati teule inaweza kuongeza utete ndani ya serikali na CCM

No comments:

Zilizosomwa zaidi