Mchakato wa kumng’oa madarakani Spika wa Bunge, Anne Makinda
ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla (CCM),
huenda usifanikiwe kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo kupingwa na
baadhi ya wabunge wenye ushawishi mkubwa katika Bunge.
Wabunge wameanza kumpinga hadharani kuhusu suala
hilo ambalo jana mjadala wake uliyateka makundi ya wabunge waliokuwa
wakihudhuria vikao vya kamati mbalimbali wakati wakiwa kwenye mapumziko.
Katika viwanja vya Bunge jana, gazeti hili
liliwashuhudia Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na swahiba wake
kisiasa, Kangi Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) wakikataa
kusaini karatasi waliyopelekewa kuunga mkono kung’olewa kwa Spika.
Baadaye kwa nyakati tofauti walisema “hoja hiyo haina mashiko” na kwamba hawakutumwa na wapigakura wao kuwania posho bungeni.
Wabunge hao walikuwa wakirejea moja ya hoja za Dk
Kigwangalla kwamba Makinda amekiuka kanuni kwa kuidhinisha malipo ya
Sh430,000 kama posho kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti
na wajumbe wa kamati nyingine ambao malipo yao ni Sh180,000 kwa siku.
Wengine wanaompinga Kigwangalla ni Mbunge wa
Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) na yule wa Kigoma Kusini, David
Kafulila (NCCR - Mageuzi), ambao pia walisema hawaoni sababu za msingi
za kumwondoa Makinda madarakani.
Rage kwa upande wake alisema haoni sababu za
msingi za kutaka kumwondoa madarakani Makinda, wakati Kafulila alisema
hilo ni suala la WanaCCM, kwani hata Spika aking’olewa atakayeziba pengo
hilo hawezi kutoka upinzani.
“Kama akitoka Makinda ataingia mtu wa opposition
(upinzani) yeyote basi ningeweza kusaini, lakini ninachojua ni kuwa kama
wakifanikiwa kumtoa watakaa kwenye Party Caucus (kikao cha chama) na
watateua mwingine kutoka miongoni mwao na mimi simwamini mbunge yeyote
wa CCM,” alisema Kafulila.
Kwa upande wake Filikunjombe alisema hoja ya Dk
Kigwangalla imejengwa katika msingi hafifu na kwamba “haizingatii
masilahi mapana ya nchi, bali masilahi binafsi kwa mtazamo finyu wenye
lengo la kujitafutia umaarufu”.
“Bunge ni taasisi kubwa ambayo haiwezi tu kuingia
katika mtego wa kuenguana kwa sababu ya posho. Watu wa Ludewa
watanishangaa leo hii wakisikia kwamba eti nimesaini kumwondoa Spika
madarakani kwa sababu ya posho,” alisema Filikunjombe na kuongeza: “Kama
hoja ingekuwa ni kumtoa Spika kwa sababu anaipendelea na kuitetea
Serikali bungeni kana kwamba yeye ni waziri, basi hoja kama hiyo mimi
ningeweza kuiunga mkono, lakini siyo suala la posho”.
Kuhusu hoja kwamba Spika Makinda alikiuka kanuni
kwa kumteua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Bajeti badala ya kuchaguliwa kwa kura, Filikunjombe alisema
wanaopaswa kulalamika kwanza ni wajumbe wa kamati hiyo na siyo mtu
mwingine yeyote.
Kwa upande wake Lugola alisema msingi wa hoja ya Dk Kigwangalla
ni masilahi binafsi na kwamba ni mapambano ya kuwania kupata kiwango
kikubwa cha posho, suala ambalo kwa sasa siyo ajenda ya kitaifa.
“Kama kweli mtoa hoja angekuwa ana nia ya dhati na
uchungu wa nchi hii, angetuunga mkono katika hoja ya kutaka kumwondoa
Waziri Mkuu, lakini hakufanya hivyo sasa iweje leo anataka tumuunge
mkono katika masuala ya posho?” alihoji Lugola.
Wabunge hao walisema fedha wanazipenda, lakini
siyo kipaumbele katika kutekeleza yale waliyotumwa na wanaowawakilisha
bungeni. Hata hivyo Dk Kigwangalla aliwapuuza wabunge hao akisema kuwa
anayetaka asaini na asiyetaka asisaini na siyo kumshambulia na kumbeza.
Vikwazo vingine
Mchakato wa kutaka kumg’oa Spika pia unaweza hata
usifike katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na badala
yake kuishia Ofisi ya Katibu wa Bunge ambako bado hoja yake inafanyiwa
kazi na wataalamu wa ofisi hiyo.
Hadi jana mchana Dk Kigwangalla alikuwa bado
hajapokea majibu kutoka ofisi ya katibu huyo na aliliambia gazeti hili
kuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alimwarifu kuwa “wataalamu
walikuwa bado wanaifanyia uchambuzi hoja yake hiyo”.
Dk Kashililah kwa upande wake aliliambia Mwananchi
Jumapili kuwa: “Ni kweli hoja yake (Dk Kigwangalla) tumeipokea na
tunaifanyia kazi, tukimaliza tutamwarifu matokeo ya uchambuzi wetu”.
Wakati Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akisubiri majibu
kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge, alisema tayari alikuwa amekusanya
saini za wabunge wapatao 110 ambao wanamuunga mkono katika harakati
zake.
Miongoni mwa hoja za mbunge huyo ni kwamba Spika
amekuwa akivunja masharti ya Kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya
kuwasilisha na kujadili jambo la dharura kwa kuzuia mijadala hiyo.
Hata hivyo hatua ya Spika Makinda kuruhusu
mijadala kuhusu migogoro baina ya wakulima na wafugaji na ile inayohusu
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili juzi, inaweza kutumika kama
kigezo cha kuiweka kando hoja ya Dk. Kigwangalla.
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema
katika mazingira hayo, Ofisi ya Katibu wa Bunge inaweza kutumia sababu
hiyo pamoja na nyingine za kiufundi kuiweka kando hoja mbunge huyo, na
kuzuia isipelekwe katika kamati husika kama kanuni zinavyoelekeza.
Kikwazo kingine ni ukimya wa Kambi ya Upinzani
Bungeni ambayo hadi sasa imekaa kimya, ikiwa ni dalili ya kuwaacha CCM
“waumane” wao kwa wao.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment