Thursday, October 17, 2013

WAZEE WA YANGA WAAHIDI USHINDI JUMAPILI HII

Ibrahim Akilimali - katibu baraza la wazee akiongea na waandishi wa habari

Viongozi wa matawi mbali mbali ya Young Africans jijini Dar es salaam pamoja na Baraza la Wazee wa klabu kwa pamoja leo wameahidi ushindi mnono siku ya jumapili katika mchezo wa jumapili dhidi ya watani wa Jadi Simba SC katika uwanja wa Taifa.
Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu, katibu wa baraza la wazee wa klabu ya Yanga Ibrahim Akilimali amesema wanashukuru viongozi kazi zao wamemaliza, makocha na wachezaji pia wamemaliza na sasa wao wanamalizia kazi ili kunogesha ushindi huo.
"Yanga tuna tamaduni zetu, sehemu yoyote ile ina asili yake, hivyo kwa hivi sasa sisi wazee kwa pamoja tunaahidi lazima tumchinje mnyama siku ya jumapili, uwezo na nia tunao hivyo washabiki wa Yanga mje kwa wingi uwanja Taifa kuishangilia timu yao" alisema Akilimali. 
Aidha Akilimali alisema kwa hivi sasa hawana wasi wasi na kikosi chao, watani wetu wanaweweseka kuona speed yetu ni yali ya juu, tunachoomba ni waamuzi kuchezesha soka kwa kufuata kanuni 17 za mchezo na kama watafanya hivyo basi lazima tumchape mnayma siku ya jumapili.
Naye kiongozi wa tawi la Temeke Kati Bakili Makele akiongea kwa niaba ya viongozi wa matawi, alisema msimu huu Yanga imejipanga vizuri na wana uhakika wa kupata ushindi siku ya jumapili kutokana na kuwa na kikosi bora.
Sisi hatutaki magoli ya kupewa kama wenzetu, mechi zote wanapewa penati, sisi tunataka kushinda ki halali kwa kufuata sheria 17 za soka, tunaamini kwa jinisi tulivyojiandaa na hali inayoendelea kwa kufuata mila na desturi ni lazima mnyama achinjwe siku ya jumapili. 
Kikosi cha Young Africans kinaendelea na mazoezi kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo wa siku ya jumapili dhidi ya Simba SC ambapo mpaka baada ya mazoezi ya leo hakuna mchezaji majeruhi hata mmoja na wote wako fit kwa ajili ya mchezo.

No comments:

Zilizosomwa zaidi