Tuesday, September 3, 2013

MAJINA YA WABUNGE WANAOHUSIKA NA KUUZA UNGA WAMO WA CCM NA CHADEMA



Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Kigwangallah, amesema amepokea majina ya wabunge, viongozi wa serikali na wafanyabiashara maarufu nchini ambao ni mapapa wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, Dk. Kigwangallah ambaye amepania kuwataja bungeni watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu, amesema baada ya kukabidhiwa majina hayo kutoka kwa wananchi, anafanya uchunguzi na kupata ushahidi ili kujiridhisha kabla hajachukua hatua ya kuwataja.

Miongoni mwa majina ya wabunge aliyopewa wamo kutoka CCM na Chadema, na wafanyabiashara maarufu wote wanatoka mkoa wa Dar es Salaam.

“Nawashukru wananchi wamenipa ushirikiano hadi jana wamenikabidhi majina ya watu saba ambao ni wabunge wawili, kiongozi mmoja mwandamizi wa serikali na wafanyabiashara wanne, ambao wote ni mapapa wauza unga na siyo madagaa,” alisema Dk. Kingwangallah.

Alisema katika kuhakikisha anatekeleza alichoahidi amemwandikia barua Spika wa Bunge kumuomba atoe maelezo kwa kuwataja majina vigogo wanaojihusisha na dawa za kulevya na kwamba bado anasubiri kujibiwa.

Dk. Kigwangallah amekabidhiwa majina hayo siku chache tu baada Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), William Lukuvi, kulieleza Bunge kuwa kama serikali itaamua kutaja wanaojihusisha na biashara hiyo hakuna atakayesalimika ndani ya bunge kwa sababu pia wamo wabunge wanaotajwa.

No comments:

Zilizosomwa zaidi