Saturday, January 19, 2013

MSHITAKIWA WA EPA AJIUA KWA RISASI


MSHITAKIWA Katika kesi ya wizi wa zaidi ya Sh bilioni tano za Benki Kuu ya Tanzania kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA), Jai Somani amejiua kwa kujipiga risasi.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kujiua jana asubuhi nyumbani kwake katika mtaa wa Mindu, Upanga katika Manispaa ya Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Parang Somani ambaye ni kaka yake, hajui kwanini mdogo wake amejiua lakini hapo awali Jai alikuwa akisumbuliwa na tatizo la msongo wa mawazo.
Jai alikuwa anakabiliwa na kesi hiyo pamoja na kaka yake Ajay Somani ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela pamoja na kulipa faini ya Sh milioni 400 baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya wizi wa Sh bilioni 2.2 kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia akaunti ya EPA.
Jai, Ajay na washitakiwa wengine wanne wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kesi hiyo bado inaendelea. Parang alisema maandalizi ya maziko yanaendelea nyumbani kwa marehemu katika mtaa wa Mindu.
Akizungumza na Habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha Jai kujiua na kuwa polisi wanaendelea na upelelezi wa chanzo cha kifo chake kwa kuwa hajacha ujumbe wowote.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka matano ya kula njama, kughushi, kuwasilisha hati ya kuhamisha deni iliyoghushiwa, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kujipatia ingizo la kiasi hicho cha fedha kutoka BoT.

No comments: