Monday, January 21, 2013

GARI LA SERIKALI LANASWA LIKIWA NA PEMBE ZA NDOVU ARUSHA

 
GARI aina ya Toyota VX linaloelezwa kuwa mali ya Serikali limekamatwa na polisi likiwa limebeba pembe za ndovu.
Gari hilo lilikamatwa juzi saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Kigongoni katika Mji wa Mto wa Mbu, wilayani Manyara baada ya gari hilo kupinduka.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya Jeshi na Polisi zimeeleza kuwa askari wa jeshi hilo aliyekuwa akiendesha gari hilo anashikiliwa na polisi.
Uchunguzi umebainisha kuwa ndani ya gari hilo kulikuwa na meno ya tembo na watu wengine watatu ambao walikimbilia porini na baadhi ya nyara hizo.
Habari hizo zimedai bado kuna utata kuhusu gari lililokuwa likitumiwa na maofisa hao kwa kuwa kibao cha namba za gari hilo kinasomeka kwa namba za kiraia lakini vioo vimechorwa namba za Serikali, huku Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa akisema pia kulikuwa na namba za JWTZ.
Kulingana na taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kukamatwa kwa gari hilo kulitokana na Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Hifadhi ya Ziwa Manyara kudokezwa na raia wema.
Inaelezwa kuwa baada ya askari hao kudokezwa, walianza kufuatilia nyendo za maofisa hao ndani ya hifadhi na walipogundua wanafuatiliwa, gari hilo liliongeza mwendo kuelekea Mji wa Mto wa Mbu.
Hata hivyo, kutokana na mwendokasi wa gari hilo na kutokuwa wazoefu kulinganisha na Askari wa Tanapa, gari la maofisa hao lilipinduka lilipofika Kijiji cha Kigongoni nje kidogo ya Mto wa Mbu.
“Baada ya kupekuliwa lilikutwa na pembe mbili za ndovu na uchunguzi wa awali umethibitisha maofisa waliokimbia walifanikiwa kutoroka na pembe nyingine tatu,” kilidokeza chanzo hicho.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kulitokana na wananchi kumtilia shaka yeye na wenzake gari lao lilipopata ajali kwa kitendo cha watu wawili waliokuwepo kwenye gari hilo kuonekana wakihamisha mizigo  na kukimbilia porini.
“Matairi mawili ya gari yalipasuka lakini ajabu ni kwamba wananchi walipojitokeza kusaidia majeruhi, wawili kati yao walinyanyua mizigo isiyojulikana na kukimbilia porini huku wakimwacha mwenzao aliyevaa sare za jeshi akisubiri garini,” alisema mtoa taarifa wetu.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati wa ajali hiyo, mtuhumiwa alikuwa amevaa jaketi la JWTZ pamoja na suruali ya jinsi akiwa na bunduki aina ya Rifle.
Katika msako uliofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi, pembe mbili zaidi  za ndovu zilikutwa zikiwa zimefichwa karibu na eneo la ajali.
Mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema hana taarifa kamili kwani yuko Tanga na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
“Ni kweli nimearifiwa juujuu tu, nasubiri taarifa kamili lakini nimeambiwa tu hilo gari lilipinduka wakati wakifukuzana na askari wetu, lakini mnaweza mkapata taarifa zaidi polisi,” alisema Kijazi.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema hajapata taarifa hiyo, hivyo asingeweza kutolea maoni kwa namna yeyote.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Zilizosomwa zaidi