Tuesday, May 14, 2013

AJALI IMETOKEA MCHANA WA LEO HUKO MBEYA WATATU WAFARIKI PAPO HAPO

JINAMIZI  LA AJALI LINAZIDI KUIKUMBA MBEYA WATU WATATU  WAMEFARIKI PAPO HAPO BAADA YA ROLI LA KAMPUNI YA KICHINA LILILOKUWA LIMEBEBA KIFUSI KUKATIKA BREKI NA KUPINDUKA MAENEO YA MWANSEKWA BARABARA YA CHUNYA MCHANA WA SAA 7 MPAKA SASA MAITI MBILI ZIMETAMBULIWA NA MOJA IMEHARIBIKA VIBAYA SANA KIASI CHA KUSHINDWA KUTAMBULIWA 
BAADHI YA WACHINA WANAOTENGENEZA BARABARA YA CHUNYA WAKIWASIKILIZA WANANCHI WALIOSHUHUDIA AJALI HIYO IKITOKEA
BAADHI YA MAJERUHI WAKISUBIRI KUPATA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA  MPAKA TUNA TOKA HOSPITALINI HAPO TUMEACHA MAJERUHI WATANO WAKIENDELEA KUPATA MATIBABU

P0LISI 16 WASHIKILIWA KWA MAGENDO JIJINI DAR


Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata askari wake 16 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kushiriki na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa magendo wanaovusha bidhaa zao kupitia bandari bubu kandokando ya Bahari ya Hindi na maeneo mengine.
Hatua hiyo umekuja baada ya kubaini baadhi ya askari wa vikosi mbalimbali ambao imeelezwa kuwa wametengeneza mtandao huo ulioanzishwa zaidi ya miezi sita kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao hukusanya fedha kinyume cha sheria kutoka kwa wafanyabiashara wasiotaka kulipa ushuru halali Serikalini.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: "Tumeshirikiana na wananchi kwa kufuatilia nyendo za askari hao na kubaini kuwa walitengeneza mtandao huo wa kuvusha mali kupitia bandari bubu zisizo rasmi maeneo ya Kawe hadi Bagamoyo."
Alisema polisi kupitia teknolojia ya kisasa iliwabaini askari hao kwa nyakati mbalimbali wakishirikiana na wafanyabiashara hao ambao walikuwa wakitoa rushwa ili wasikamatwe.
“Mpaka sasa askari wa vyeo mbalimbali waliokamatwa wako 16 na wanaendelea kuhojiwa... majina yao yanahifadhiwa kwa sasa kwani bado kuna wengine wanatafutwa ili kuwabaini na kuusambaratisha mtandao mzima,” alisema.
Alisema mtu yeyote ambaye amefanya kosa ndani ya Jeshi la Polisi atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani kama raia wengine.
Kamanda Kova alisema operesheni hiyo itawalenga wafanyabiashara, wafanyakazi wa TRA na wa taasisi nyingine watakaobainika kuhusika na mtandao huo.

HII NI NYINGINE KWA WENYE MABASI KUTAKA NAULI IPANDE TENA


BAADHI ya wamiliki wa mabasi mkoani Shinyanga, wamesema asilimia 24.46 iliyoongezwa katika nauli haitoshi.
 
Wamiliki hao wameyasema hayo ikiwa ni takriban mwezi mmoja tangu kuanza kutumika kwa nauli mpya za usafiri wa barabara, reli na kupandishwa kwa tozo za huduma za meli bandarini.


Hatua hiyo ilichukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Aprili 3 mwaka huu.

Wakizungumza na Mtanzania kwa nyakati tofauti mjini Shinyanga, baadhi ya wamiliki wa mabasi na wadau wa sekta ya usafirishaji nchi kavu, walisema awali wao waliwasilisha mapendekezo yao kwa SUMATRA wakiomba kupandishwa kwa nauli kwa asilimia 149.

Mmoja wa wamiliki wa mabasi ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake , alisema kutokana na kupanda kwa bei ya spea za magari na gharama za uendeshaji, kampuni nyingi kwa sasa zinashindwa kufanya matengenezo ya mabasi yao.

Alisema katika mwaka mmoja uliopita, tairi ya gari kubwa ilikuwa ikiuzwa Sh 400,000 lakini kwa sasa inauzwa Sh 650,000.

Wakati huo bima ilikuwa Sh 450,000 lakini sasa imepanda hadi Sh 1,000,000, alisema.

Alitaja gharama nyingine kuwa ni kodi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ushuru wa kituo cha mabasi Sh 2,000 na ada ya Chama cha Madereva Sh 5,000 ambazo hutozwa kwa kila basi linaloingia katika kituo cha mabasi.
Chanzo Mpekuzi

HAYA NDIO MAJIBU YA IKULU KWA DR. SLAA KUHUSU KASHFA YA UDINI WA RAISI KIKWETE ALIZOZITOA


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Wilbroad Slaa, leo, Jumatatu, Mei 13, 2013, amekaririwa na gazeti moja akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni, “ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa Serikali nataifa” kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Aidha, katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Dk. Slaa amlipua JK” kwenye gazeti linalounga mkono CHADEMA la Tanzania Daima,Mheshimiwa Slaa anadai kuwa migogoro ya sasa ya kidini “inajengwa au kutengenezwa na Serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika misikiti wakati wa kampeni za Urais mwaka 2010”.

Kwa hakika, hakuna namna nyingine ama namna bora zaidi ya kuielezea kauli hii ya Mheshimiwa Slaa isipokuwa kwamba kauli hiyo ni riwaya nyingine isiyokuwa na mshiko. Ni uongo mtupu. Yake Mheshimiwa Slaa ni maneno yasiyokuwa na ukweli wowote.

Ni uzushi na santuri ambayo imezoeleka sasa kwa wananchi. Kauli ya Mheshimiwa Slaa ni mwendelezo wa mtiririko usiokuwa na mwisho wa ghiriba ambazo kamwe hazitafanikiwa za Mheshimiwa Slaa kuwahadaa wananchi ukweli wa mambo ulivyo katika nchi yetu. 



Rais Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni kamwe hawakufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, ama wa mwaka mwingine wowote, katika nyumba yoyote ya ibada iwe msikitini ama kanisani ama hekaluni ama nyumba nyingine yoyote ya ibada mahali popote katika nchi yetu.

Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi hata kufikiria kuchanganya dini na siasa. Hana sababu ya kufanya hivyo. Anaelewa fika madhara ya udini kwa mustakabali wa nchi yetu, kwa umoja wa taifa letu na kwa mshikamno wa wananchi wake.

 
 Yoyote anayejaribu kumbebesha Rais Kikwete msalaba wa udini ana lake jambo na ni vyema atuambie fika Rais alitumia Msikiti upi, ama Kanisa lipi, mahali gani na kwa nyakati gani kufanya kampeni. 

Vinginevyo, kauli ya Mheshimiwa Slaa itabakia ni kauli tu inayostahili kupuuzwa na wananchi, itabakia ni kauli ya mtu mzima anayetapatapa na kufanya jitihada kubwa kujivunjia mwenye heshima kwa kutunga na kusambaza uongo.

Tunanapenda kumshauri Mheshimiwa Slaa kuwa kama  hana jambo la maana lakuwaambia wananchi ama ameishiwa na hoja ni vyema  anyamaze, awaachie wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo, kuliko kuendeleza riwaya zake zisizokuwa na mshiko.Yake ni santuri iliyowachosha wananchi.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Raisi Ikulu.
Dar es Salaam.
13 Mei, 2013

Zilizosomwa zaidi