Sunday, March 24, 2013

TAIFA STARS YAENDELEA KUFANYA VIZURI KATIKA KUFUZU KUCHEZA KOMBE LA DUNIA 2014.

Mabao matatu ya nyota wa TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu yalitosha kuipa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Morocco katika mechi ya kutafuta tik-eti ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia, Brazil 2014.

Kwa ushindi huo, Stars sasa imefikisha pointi sita na hivyo kuendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C ikiwa nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, baada ya kuifunga Gambia mabao 3-0 juzi.
Mshambuliaji Ulimwengu aliyeingia akitokea benchi kipindi cha pili alifunga bao la kwanza la Stars dakika ya 46, kabla ya kumtengenezea nyota mwenzake wa TP Mazembe, Samata aliyefunga mengine mawili dakika ya 66 na 80.

Stars ilianza mchezo huo kwa kasi na kulifikia lango la wapinzani wao dakika ya pili tu ya mchezo wakati shuti la kiungo Amri Kiemba ilipogonga mtambaa wa panya kabla ya mabeki wa Morocco kuon-doa mpira kwenye hatari.

Dakika ya tisa Morocco ilijibu mapi-go na kona iliyochongwa na Barrada Abdellaziz ilimfikia Abuurazouk Hamza ambaye alipiga kichwa kilichotoka senti-mita chache kwenye lango la Stars.

Baada ya kashikashi hizo, kila upande ulijaribu kutuliza mpira chini na kupelekeana mashambulizi kwa zamu. Hata hivyo hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika hakuna timu ili-yokuwa imetingisha nyavu.

MAANDAMANO CHADEMA SASA BASI...!

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekubali kusitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike leo kushinikiza kujiuzulu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012.

Makubaliano yalifikiwa baada ya kikao cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema na viongozi wa Chadema walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kilichofanyika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

MVUA YASABABISHA MAFURIKO TENA DAR.

Mvua kubwa iliyonyesha jana jijini Dar es Salaam, ilisababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya maeneo, hivyo nyumba kadhaa kujaa maji na baadhi ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua iliyoanza kunyesha muda wa asubuhi, pia yalisababisha hasara kubwa kutokana na vitu na mali mbalimbali kusombwa na maji.
Barabara kadhaa zilikuwa hazipitiki kutokana na kujaa maji, huku baadhi ya nguzo za umeme na simu ambazo zilikuwa karibu na mifereji ziliharibiwa na kusombwa na maji.

Athari kubwa ya mafuriko hayo ilitokea katika eneo la Kigogo Darajani ambako baadhi ya nyumba zilikuwa zimejaa maji na baadhi ya vitu vilionekana vikielea kwenye mikondo mikubwa ya maji.
Mmoja wa waathirika hao, Andrew Simon (35) alisema nyumba yake ilijaa maji kwa takriban futi nne kwenda juu na kusababisha hasara ya mali ambayo alikuwa bado hajafahamu thamani yake.

MULUGO AKUMBWA NA KASHFA YA VYETI...ISOME HAPA STORI KAMILI.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.

Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan. 

Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”

Waliomfundisha
 Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
CHANZO: MWANANCHI

TAARIFA RASMI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, MHE. XI JINPING NCHINI, TAREHE 24 – 25 MACHI 2013 ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHE. BERNARD K. MEMBE

 

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza na Waandishi wa
Habari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya
kitaifa ya siku mbili ya Rais mpya wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi
Jinping atakayoifanya hapa nchini kuanzia tarehe 24 hadi 25 Machi, 2013.
Wengine katika picha ni Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) (kulia), Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Bw. John Haule, Katibu Mkuu wa Wizara  wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 Mhe. Membe, Mhe. Maalim, Bw. Haule na
Balozi Gamaha wakisikiliza swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo
pichani) wakati wa mkutano kuhusu ziara ya Rais wa China, Mhe. Xi
Jinping hapa nchini.
 Mmoja wa waandishi wa habari kutoka
China akiuliza swali kwa Mhe. Membe (hayupo pichani) wakati wa mkutano
kuhusu ziara ya Rais wa China hapa nchini
 Waandishi kutoka mashirika mbalimbali ya habari ya China pia walikuwepo kwenye mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajab Gamaha (kulia) akiwa na
Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Philip Marmo (katikati) pamoja na
Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Bertha Semu-Somi wakimsikiliza Mhe.
Membe (hayupo pichani) alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara
ya Rais wa China hapa nchini
---
TAARIFA RASMI KUHUSU ZIARA YA RAIS
WA JAMHURI YA WATU WA CHINA, MHE. XI JINPING NCHINI, TAREHE 24 – 25 MACHI 2013
ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHE. BERNARD
K. MEMBE (MB), TAREHE 22 MACHI 2013
 
---



1.0     UTANGULIZI

1.1     Ndugu waandishi, nimewaita leo ili
kuwaeleza kuhusu ziara ya kihistoria hapa nchini ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China, Mhe. Xi Jinping ambayo itafanyika hivi karibuni. Najua mtakuwa
mmekwishasikia kuwa Rais huyu atafika nchini hivi karibuni.
Sasa
niwatangazie rasmi kuwa taarifa hii ni sahihi na ziara hiyo itafanyika tarehe
24 – 25 Machi, 2013. Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Xi barani Afrika mara tu
baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo ya Urais mnamo tarehe 14 Machi, 2013.
1.2     Mahusiano
ya  Tanzania na China yametoka
mbali, tangu enzi ya waanzilishi wa mataifa haya mawili, yaani Mwalimu Julius
Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong  wa
China. Ifahamike kuwa, kutokana na mahusiano haya ndipo mmoja ya miradi mikubwa
kabisa iliyofanywa na China barani Afrika ulitokea. Mradi huu ni reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA). Pamoja na kuwa mradi wa kimaendeleo, reli hii ya
TAZARA ilitusaidia katika ukombozi wa bara la Afrika – kama moja ya njia za
usafiri, hivyo kuifanya China kuwa rafiki wa kweli. Mradi mwingine mkubwa ni
ujenzi wa jengo la Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia. Haya, kati ya
mengineyo, yanafanya ugeni huu kuwa wa kihistoria na heshima kubwa kwetu.
 1.3    Rais
Xi anakuja kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete na akiwa nchini atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Mheshimiwa
Rais Kikwete, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.
Dkt Ali Mohamed Shein. Mheshimiwa Xi ataambatana na mke wake, pamoja na Maafisa
Waandamizi wa Serikali ya China wasiopungua 25.
2.0     RATIBA YA MGENI KWA KIFUPI
2.1     Rais Xi Jinping atawasili nchini siku ya
jumapili tarehe 24 Machi, 2013 saa 10:25 jioni katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege maalumu aina ya Boeing 747 ambapo
atalakiwa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
2.2     Baadaye Rais Xi pamoja na ujumbe wake
watafanya mazungumzo rasmi na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi
wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazungumzo hayo yataanza saa
12:15 jioni na yatafanyikia Ikulu.
2.3     Baada ya mazungumzo rasmi, Rais Xi pamoja
na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano
na Mikataba mbalimbali (kumi na tisa) ya ushirikiano baina ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania/na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa upande mmoja na Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China kwa upande mwingine. Kwa kifupi mikataba hiyo inahusu kukuza
uwekezaji na biashara baina ya nchini za Tanzania na China, kukuza ushirikiano
wa kiutamaduni baina ya nchi hizi mbili na watu wake, nk.
2.4
    Baada ya tukio hilo, Rais Xi pamoja na
ujumbe wake watahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa  kwa heshima yake na Rais Jakaya Kikwete.
Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 1:40 usiku. Hilo ndilo litakuwa tukio
la mwisho kwa siku ya kwanza.
2.5     Siku itakayofuata ya tarehe 25 Machi, 2013
saa 3:10 asubuhi Rais Xi atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa
Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
2.6     Tukio litakalofuata litakuwa ni uzinduzi na
makabidhiano rasmi ya kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kwa lengo la
kumuenzi Mwalimu Nyerere. Baada ya makabidhiano ndipo Rais Xi atatoa hotuba
maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Hotuba hiyo itajikita katika
kuelezea Sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika. Watu kutoka kada mbalimbali
kama vile Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, Wanafunzi, Wabunge, Viongozi na Maafisa
Waandamizi wa Serikali, Wafanyabiashara, n.k. wamealikwa kuhudhuria ukumbini
hapo.
2.7     Mchana wa tarehe 25 Machi, 2013 Rais Xi
Jinping ataelekea katika Makaburi ya Wataalamu wa Kichina ya Majohe yaliyopo
katika kijiji cha Majohe – Ukonga ambapo atatoa heshima zake kwa Wachina
waliofariki wakati wakijenga Reli ya TAZARA.
2.8     Baada ya hapo Rais Xi ataelekea Uwanja wa
Ndege wa Julius K. Nyerere ambapo ataondoka saa 10:40 jioni kuelekea nchini
Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi za BRICS.
3.0     FAIDA
ILIYOPATA TANZANIA KUTOKANA NA UHUSIANO NA CHINA
3.1     Jambo kubwa Tanzania inalojivunia tangu
kuanzisha uhusiano na China ni kukua kwa urafiki wa karibu sana na China;  urafiki wa kuaminiana na kusaidiana katika
nyanja mbalimbali za kitaifa, kikanda na kimataifa. Uhusiano huo wa karibu
unazidi kukua kila kukicha.
3.2     Kwa upande wa ushirikiano wa kiuchumi
Tanzania inajivunia miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa kwa
ushirikiano na China. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na:

         
i.   
Mradi
wa Reli ya TAZARA – kama nilivyoeleza hapo awali Mradi huu umekuwa mhimili na
kiungo muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani za
Zambia, DRC, Zimbabwe n.k, hususan
katika sekta ya usafirishaji wa rasilimali ghafi, bidhaa za kibiashara
na abiria
        
ii.   
Kiwanda
cha nguo cha URAFIKI – (licha ya changamoto kadhaa zinazokikabili) kiwanda hiki
kimetoa ajira kwa Watanzania wengi, pamoja na soko kwa pamba inayolimwa hapa nchini.
      
iii.   
Miradi
mikubwa ya maji ya Shinyanga, Dar es Salaam na Pwani.
       
iv.   
Viwanja
vya kisasa vya michezo – Uwanja wa Taifa (Dar es Salaam) na Karume Stadium
(Zanzibar).
        
v.   
Kituo
cha maonesho na majaribio ya zana za kilimo cha Mvomero, Morogoro.
       
vi.   
Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius K. Nyerere. Manufaa ya Kituo hiki
cha Mikutano ni kama yale yanayopatikana katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC).
     
vii.   
Mradi
wa ujenzi wa mkongo wa Taifa kwa Tanzania bara na Zanzibar – mradi huu ni
muhimu sana katika maendeleo ya sekta ya Teknohama (Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano). Manufaa yake yatapatikana si tu hapa Tanzania lakini pia kwa nchi
za jirani kama vile Rwanda, Burundi, n.k, kwani huduma hii itatolewa kibiashara.
   
viii.   
Mradi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam – Mradi huu utakapokamilika
hapo mwakani utatupatia uhakika wa umeme, pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa
gharama zake. Pia utapelekea kupungua kwa gharama za maisha kwa ujumla na kukua
kwa kipato cha mtu mmoja mmoja kiuchumi.
       
ix.   
Manufaa
mengine mengi yanatarajiwa kupatikana mara baada ya ziara.

4.0 MATARAJIO YA TANZANIA KUTOKANA NA ZIARA HII
4.1     Katika ziara hii ya kihistoria Tanzania
inatarajia kufaidika kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:
         
i.   
Kufungua
milango ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ziara hii inafuatiliwa na
kumulikwa na nchi karibu zote duniani; pamoja na makampuni makubwa kila kona ya
dunia. Ziara ya Rais wa huyu wa China inatuma ujumbe kwa wawekezaji kote
duniani kuhusu mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini
Tanzania.

        
ii. Wakati
wa ziara hii mikataba na makubaliano zaidi ya 19 yatatiwa saini kati ya
Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa upande mmoja, na Serikali ya China kwa upande mwingine (tafadhali rejea kiambatisho Na.1 kwa
orodha ya Makubaliano na Mikataba iyakayotiwa saini.)




Kama
ilivyoelezwa hapo awali, Mikataba na makubaliano haya yanagusa sekta za kilimo
kibiashara, uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu, miradi ya maji na umeme,
fursa za kimasomo kwa vijana wa Kitanzania nchini China, nk.




5.0     HITIMISHO



5.1     Uhusiano
kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu tangu miaka ya 1950 wakati bado
Tanzania (Tanganyika kwa wakati huo) ikiwa katika harakati za kupigania Uhuru.
Mwaka kesho (2014) nchi zetu mbili zitasherehekea miaka 50 ya uhusiano wa
kidiplomasia. Uhusiano huu unatoa picha ya ukaribu uliopo kati ya Serikali za
nchi za Tanzania na China pamoja na watu wake.



5.2     Hivyo basi, napenda kuchukua fursa hii
kuwaomba Watanzania wote kwa ujumla tujitokeze kwa wingi kumlaki Rais Xi
Jinping atakapokuwa anawasili kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K.
Nyerere mpaka Hoteli ya Serena atakapofikia kwa kupitia Barabara ya Pugu/Julius
K. Nyerere.

HIZI NDIO STORI KUBWA, MICHEZO NA BURUDANI KWENYE MAGAZETI YA LEO JUMATATU MARCH 25.

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

Zilizosomwa zaidi